Abstract:
Ikisiri: Lugha ni kiungo muhimu cha riwaya kwani ni kupitia kwa lugha ambapo mwandishi
huyafikia malengo yake ya kisanaa na kuwasilisha ujumbe wake. Suala hili limechangamkiwa na
watafiti wengi wa fasihi kote ulimwenguni. Makala hii inajikita katika kuchunguza mchango wa
mazingira ya mwandishi katika matumizi ya mafumbo kwenye riwaya mbili za Katama Mkangi:
Mafuta na Walenisi. Kwanza, makala hii imebainisha kuwa, wakati ambapo Mkangi alikuwa
akiandika riwaya hizi, uhuru wa kuikosoa serikali iliyokuwa mamlakani haukuwepo na kwa
hivyo, alilazimika kutumia ufumbaji kuwasilisha ujumbe wake ili kuhepa rungu ya serikali. Pili,
alikosomea na waandishi wengine, walimwathiri katika matumizi ya mbinu ya ufumbaji katika
Uandishi wake. Tatu, hali ya kisiasa dhidi ya waandishi wakati wa uandishi wake ilimlazimisha
kutumia lugha ya ufumbaji ili ichukuane na wakati huo. Aidha, kutokana na makala hii ni dhahiri
kuwa Mkangi alitumia mbinu ya ufumbaji kumzindua msomaji kuhusu athari za utabaka,
ubepari, unafiki wa viongozi miongoni mwa mengine. Yaliyoshughulikiwa katika makala hii
yalilikusanywa kupitia kwa upekuzi wa maandishi na riwaya mbili za Mkangi: Mafuta na
Walenisi kwa kuzingatia lugha ya mafumbo. Makala haya ni muhimu kwa kuwa yatawasaidia
wasomaji kuelewa kazi hizi za Mkangi zilizoandikwa kimafumbo.
Maneno Muhimu: Mafumbo (Ufumbaji), Mazingira, Lugha, Mafuta na Walenisi