Abstract:
Utafiti huu ni tathmini ya usawiri linganishi wa ushujaa katika tendi za Fumo Liyongo,
Mikidadi na Mayasa na Swifa ya Nguvumali. Madhumuni ya utafiti huu ni kumtambulisha
shujaa kwa vigezo vya ushujaa wa Kiafrika katika tendi teule za Kiswahili, kutathmini
mchango linganishi wa mazingira katika kusawiri ushujaa katika tendi teule na kubainisha
kiulinganifu matumizi ya mbinu za utunzi katika kusawiri ushujaa katika tendi teule. Uteuzi
wa mada ya utafiti uliongozwa na kuwepo kwa pengo la kiusomi. Hata ingawa tafiti nyingi
zimefanywa kuhusiana na swala la ushujaa, mtafiti hajaweza kutagusana na utafiti
uliochunguza ulinganishi wa ushujaa katika tendi teule za Utendi wa Fumo Liyongo, Utendi
wa Mikidadi na Mayasa na Utendi wa Swifa ya Nguvumali. Utafiti huu uliongozwa na
nadharia tatu. Nadharia ya kwanza ni Mithiolojia iliyoasisiwa na Raglan (1936) na Rank
(1909) na kuendelezwa na Okpewho (1979) na Mulokozi (2002). Nadharia ya Mithiolojia
imeorodhesha sifa bainifu za shujaa wa Kiafrika ambazo shujaa wa Kiafrika anafaa kuwa
nazo katika tendi. Nadharia ya pili ni Ujumi Mweusi ya Zirimu (1971). Nadharia hii
inapendekeza fasihi ya Kiafrika ihusishe Uafrika na mazingira ya Kiafrika katika kusawiri
ushujaa. Nadharia hii inalenga kuonyesha hali ya kujivunia Uafrika. Nadharia ya tatu ni
Umaumbo ya Shyklovsky ( 1904) na kuendelezwa na Roman ( 1919). Nadharia ya Umaumbo
inashikilia kuwa kazi za fasihi ziweze kuandikwa kwa sifa bainifu za umbo maalumu na
zitumie mbinu mahususi za utunzi katika kufikisha ujumbe wa kifasihi. Utafiti huu ulikuwa
wa maktabani. Maktaba mbalimbali yakiwemo ya intaneti yalitumika. Kundi lengwa la utafiti
huu, lilikuwa tendi za Kiswahili, ambapo kimaksudi mtafiti aliteua tendi tatu ambazo ni
Utendi wa Fumo Liyongo, (Kijumwa, 1913) Utendi wa Mikidadi na Mayasa, (Bashir 1972),
na Utendi wa Swifa ya Nguvumali, (Ismaili 1968). Data imeandikwa kwenye nakala ngumu
na pia kwa tarakilishi. Data ilikusanywa kwa njia ya uchanganuzi wa yaliyomo kwa
kuzisoma tendi zenyewe na kazi mbalimbali zilizohusu suala la ushujaa. Uchanganuzi wa
data ulikuwa kwa njia ya maelezo ambapo data ilieandikwa, ikachujwa na kufafanuliwa.
Matokeo ya utafiti yamewasilishwa kwa njia ya maandishi. Utafiti huu umemtambulisha
shujaa kwa vigezo vya shujaa wa Kiafrika katika tendi teule, na uligundua kuwa, si kila
shujaa wa tendi teule za Kiswahili uafiki vigezo vya kumtambulisha shujaa wa Kiafrika.
Mtafiti ametathmini mchango linganifu wa mazingira, na kuamua kuwa mazingira yana
mchango mkubwa katika kumjenga shujaa katika tendi teule za Kiswahili. Kiulinganifu,
utafiti uligundua kuwa, mbinu za utunzi zina nafasi kubwa katika kusawiri ushujaa. Mbinu
nyingi zilitumika katika tendi zote ila tu mbinu za Ndoto na Ngomezi, ambazo zilitumika
katika baadhi ya tendi. Matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kuwa ya muhimu kwa jamii ya
wasomi katika urejeleaji wa dhana ya ushujaa na kuzua mtazamo mpya wa usawiri wa
ushujaa kwa kulinganisha ushujaa katika tendi teule. Utafiti huu ni daraja kwa watafiti wa
baadaye na ni nyongeza kwa tafiti ambazo zimefanywa kuhusiana na suala la ushujaa katika
tendi za Kiswahili.