dc.description.abstract |
Mwingiliano matini ni dhana ya kuathiriana, kuhusiana na kutegemeana kwa matini. Kila matini huwa na mwingiliano kwani hurejelea, huchakata na huchota kutoka kwa matini tangulizi. Kila kazi ya kisanaa, kulingana na Kristeva, ni mwingiliano ambao huathiriana na matini nyingine, huandikwa upya, huzigeuza au huzibeza matini. Dhana hii ya mwingiliano matini iliibua haja ya uchambuzi wa tamthilia ya Kinjeketile (1969) ya Ebrahim Hussein na Majira ya Utasa (2015) ya Timothy Arege. Kuna tafiti chache ambazo zimefanywa kuhusiana na suala la mwingiliano matini katika kulinganisha kipindi cha ukoloni na nyakati za sasa baada ya ukoloni. Hivyo, kazi hii ililenga kutafiti nyanja hii ambayo haijatafitiwa vya kutosha kwa kutathmini ni kwa kiwango kipi tamthilia ya Kinjeketile inapigwa mwangwi na tamthilia ya Majira ya Utasa. Malengo yaliyoongoza utafiti huu yalikuwa: kubainisha mfanano wa muktadha wa kihistoria na kijami wa tamthilia za Kinjeketile na Majira ya Utasa, kulinganisha maudhui katika tamthilia hizi na kutambulisha mfanano wa fani katika tamthilia tulizoteua. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Mwingiliano matini ya Julia Kristeva (1986). Mihimili iliyoongoza utafiti huu ni pamoja na: matini yoyote ile ni madadiliko ya mpangilio wa matini nyingine, kazi za fasihi huundwa kutokana na mifumo ya kanuni na tamaduni mbalimbali zilizowekwa na kazi tangulizi, matini moja hufafanua usomekaji wa mkusanyiko wa matini zote za kongoo moja ambapo matini tangulizi hufyonzwa na kujibiwa na matini mpya, matini za kifasihi huchota, kunukuu, kugeuza na kuiga kwa kurejelea matini nyingine. Muundo wa utafiti huu ulikuwa wa uchanganuzi wa yaliyomo. Data ilikusanywa kutokana na usomaji wa kina wa tamthilia tulizoteua. Matokeo ya utafiti huu yalibainisha kwamba tamthilia za Kinjeketile na Majira ya Utasa zina mfanano wa muktadha wa kihistoria na kijamii wa utunzi wake. Vilevile ilibainika kuwa kuna maudhui na fani zinazolingana katika kazi hizi. Utafiti huu ni wa manufaa kwa wanafunzi wa fasihi, waandishi na pia walimu wa fasihi. Kazi hii ni matini nyingine ya kurejea haswa katika uchambuzi wa fasihi inayolinganisha kazi ya vipindi tofauti vya kihistoria na kijamii. |
en_US |