Abstract:
Utafiti huu umechunguza ufumbaji katika riwaya mbili za Katama Mkangi: Mafuta na
Walenisi. Utafiti huu umelenga: Kwanza, kubainisha aina mbalimbali za ubunifu wa
ufumbaji uliojitokeza katika riwaya ya Mafuta na Walenisi. Pili, kudhihirisha jinsi ufumbaji
ulivyotumiwa na mwandishi kama kichocheo cha zinduko katika riwaya ya Mafuta na
Walenisi. Tatu, kudhihirisha namna ufumbaji umeendeleza au kukwamiza usawiri wa
wahusika wa mtunzi. Nne, kutathimini jinsi mazingira ya mwandishi yalivyochangia
matumizi ya mafumbo katika riwaya ya Mafuta na Walenisi. Utafiti huu umebainisha kuwa,
wakati ambapo Mkangi alikuwa akiandika riwaya hizi, uhuru wa kuikosoa serikali iliyokuwa
mamlakani haukuwepo na kwa hivyo, alilazimika kutumia ufumbaji kuwasilisha ujumbe
wake ili kuhepa rungu ya serikali. Pili, alikosomea na waandishi wengine, walimwathiri
katika matumizi ya mbinu ya ufumbaji katika uandishi wake. Tatu, kutokana na kazi hii, ni
dhahiri kuwa Mkangi alitumia mbinu ya ufumbaji kumzindua msomaji kuhusu athari za
utabaka, ubepari, unafiki wa viongozi, sheria na nafasi yake katika jamii, umuhimu wa utu na
usawa, umuhimu wa mapinduzi katika ujenzi wa jamii mpya, elimu na utafiti, mchango wa
vijana katika ujenzi wa taifa miongoni mwa mengine. Aidha, imebainika kuwa Mkangi
alitumia taswira, jazanda na istiari katika kufumba ujumbe wake. Hali kadhalika,
imedhihirika kuwa ufumbaji ulimsaidia Mkangi katika usawiri wa wahusika wake kwa
kuwapa majina ya majazi na lugha ya kimafumbo. Utafiti huu umeongozwa na Nadharia
Amali ambayo hupima umuhimu wa kitu kwa kuangalia matokeo ya matumizi ya hicho kitu.
Nadharia hii hujishughulisha zaidi na matokeo na athari za hayo matokeo. Kwa hivyo,
tumechunguza umuhimu wa ufumbaji kwa kuangalia matokeo na athari zake kwenye kazi za
Mkangi. Utafiti huu ulifanyiwa maktabani na kwenye mtandao. Kwa jumla mafumbo
yamechunguzwa na kuwekwa katika makundi kutegemea namna yalivyojengwa. Ukusanyaji
wa data ulifanywa kupitia kwa mbinu ya uchanganuzi wa matini au yaliyomo. Data
iliyokusanywa na kuchanganuliwa imewasilishwa kwa njia ya maelezo. Utafiti huu ni
muhimu kwa njia mbalimbali. Kwanza, utakuwa kama mwongozo kwa waandishi wa
baadaye kuandika kazi nzuri zaidi kimafumbo. Pili, utawasaidia wasomi kuelewa kazi hizi
zilizoandikwa kimafumbo. Tatu, utafiti huu unachangia pia katika kuangalia riwaya za
Kiswahili kitaaluma hasa kwa misingi ya ufumbaji kwa kutumia Nadharia Amali.