Abstract:
Kimsingi, lugha inawezesha na kuendeleza mazungumzo katika jamii. Lugha hii hujitokeza katika mazungumzo na maandishi. Mawasiliano andishi yanatakiwa kufanywa kwa uangalifu mkubwa ili kukamilisha gharadhi lake katika jamii. Ilivyobainika ni kwamba pasipo lugha, mawasiliano kama shughuli kuu ya kibinadamu hayatafaulu. Ingawa makosa mbalimbali yanayopatikana katika kazi za wanafunzi yametambuliwa na kuchanganuliwa na wataalamu mbalimbali, bidii hazijafanywa katika kubainisha makosa ya kisemantiki katika mawasiliano andishi ya Kiswahili kwa kina. Lengo kuu la utafii huu ni kuchanganua makosa ya kisemantiki katika mawasiliano andishi ya Kiswahili miongoni mwawanafunzi wa shule za upili katika kaunti ya Kakamega. Utafiti huu umeainisha makosa yaliyojitokeza katika matini za wanafunzi wa shule za upili; kubainisha vyanzo vya makosa husika na kupendekeza mbinu mwafaka za kuyapunguza. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Uchanganuzi Makosa pamoja na Nadharia ya Sarufi Zalishi. Sampuli ya kitabaka ilitumiwa kuteua shule kumi na mbili za upili na wanafunzi kumi wa kidato cha tatu kutoka kila shule, katika kaunti ya Kakamega ili kufanikisha utafiti huu. Idadi lengwa ya wanafunzi ni mia moja ishirini.Tulikusanya data kutoka nyanjani. Utafiti huu ulitumia hojaji na mjarabu. Watafitiwa walitunga sentensi na kuandika matini yenye maneno kati ya mia mbili na mia mbili hamsini. Data zote zilichambuliwa na kuwasilishwa kwa maelezo na utumiaji wa jedwali kwa shabaha ya kuonyesh auhusiano wake na malengo ya utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu yalibainisha kuwa makosa ya kisemantiki yalijitokeza katika matini za watafitiwa.Vyanzo vya makosa vilijadili wa na kuwekwa wazi. Kuhusu mbinu za kupunguza utokeaji wa makosa katika matapo husika, utafiti huu ulipendekeza mbinu mbalimbali za kuzingatiwa kwa kina. Matokeo ya utafiti huu yametoa mwanga kwa walimu wa Kiswahili, wanafunzi wa shule za upili na Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala kuhusu mbinu za kutumia katika kupunguza makosa ya kisemantiki yanayojitokeza katika matini za watafiti husika. Pia, utafiti huu umependekeza masuala ambayo yanaweza kushughulikiwa kwa kuwa hayakushughulikiwa katika utafiti huu.