Abstract:
Utafiti huu unahusu tathmini ya matumizi ya lugha katika uwasilishaji wa habari za
mazingira katika gazeti la Taifa Leo nchini Kenya. Gazeti la Taifa Leo huwasilisha habari
kwa wasomaji kwa lugha ya Kiswahili. Lugha ya Kiswahili inatambuliwa na Katiba ya
Kenya kama lugha ya taifa na pia lugha rasmi sambamba na lugha ya Kiingereza.
Mazingira ni suala mtambuko na nyeti kitaifa na kimataifa. Mazingira yanaathiri maisha
ya kila kiumbe kila siku kwa njia moja au nyingine. Inatarajiwa kwamba, kwa vile vyombo
vya habari, Gazeti la Taifa Leo likiwemo, vimetwikwa jukumu la kuwapasha wanajamii
yale yanayoendelea duniani kuhusiana na mazingira, vitafanya hivyo kwa namna ambayo
itawawezesha watu kufahamu umuhimu wa mazingira na hivyo kuingiliana nayo kwa njia
chanya. Hoja hii inatokana na imani kwamba mtu huthamini na kutunza kile anachofahamu
thamani yake. Uchunguzi huu ulinuia kubainisha iwapo matumizi ya lugha katika kueleza
habari za mazingira kwenye gazeti la Taifa Leo hufanikisha mawasiliano. Uchunguzi huu
ulidhamiria kutimiza malengo yafuatayo: kuchanganua vipengele vya lugha
vinavyoteuliwa na waandishi wa habari katika kuripoti habari za mazingira katika gazeti
la Taifa Leo, kutathmini mtindo wa uwasilishaji wa habari za kimazingira na kubainisha
ujumbe uliowasilishwa na waandishi wa habari katika gazeti la Taifa Leo. Nadharia
zilizotumika katika utafiti huu ni Nadharia ya Uchanganuzi Usemi (NUU) iliyoasisiwa na
Michel Foucault (1928) na baadaye ikaendelezwa na Norman Fairclough (1989) na
Nadharia ya Umtindo (NU) ambayo iliasisiwa na Geoffrey Leech (1965-1966) na
ikapaliliwa na Simpson (2004). Utafiti huu ulifanyika maktabani ambapo taarifa kuhusu
habari za mazingira zilizochapishwa katika gazeti la Taifa Leo zilichanganuliwa. Magazeti
ya Taifa Leo yaliyochapishwa kuanzia Januari 2021 hadi Machi 2022 yaliteuliwa kwa
kudhamiria, hususan yale yaliyokuwa na habari kuhusu mazingira. Data ilikusanywa kwa
kudondoa matumizi ya lugha, mtindo uliotumiwa katika uwasilishaji wa taarifa za
mazingira kutoka magazeti ya Taifa Leo teule pamoja na aina na dhima za ujumbe
uliojitokeza katika habari hizo. Utafiti huu ulichanganua matini 270 kutoka kwa magazeti
ya Taifa Leo yaliyoteuliwa kimaksudi. Matini hizi ni zile ambazo zilifafanua taarifa
zinazohusiana na mazingira. Data iliyokusanywa katika utafiti huu ilikuwa ya kithamano.
Data ya kithamano ilikuwa zile habari zilizofafanua masuala ya mazingira katika gazeti la
Taifa Leo. Data ya kithamano ilichanganuliwa kwa njia ya maelezo kwa kuzingatia
mihimili ya nadharia teule. Matokeo ya utafiti yaliwasilishwa kwa maelezo, jedwali na
takwimu. Inatarajiwa kwamba matokeo ya utafiti huu yatafaidi wanafunzi, watafiti,
wanaharakati wa kimazingira, taaluma za Uchanganuzi Usemi, Umtindo na Pragmatiki,
wanahabari, wachapishaji wa habari katika magazeti, na wasomaji wa habari hizo.
Umuhimu wa Kiswahili kama wenzo wa mawasiliano pia umeangaziwa.