Abstract:
Utafiti huu ulishughulikia muundo na ruwaza ya kivumishi cha lahaja ya Kiimenti
kinapotumika katika tungo za Kiimenti. Kiimenti ni lahaja mojawapo ya lugha ya Kimeru
inayozungumzwa katika kaunti za Meru na Tharaka Nithi. Lahaja hii haijafanyiwa utafiti
mwingi. Kwa hivyo, utafiti huu ni jitihada za kuongezea maarifa katika lahaja hii.
Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa kubainisha aina za vivumishi katika lahaja ya
Kiimenti; kuchunguza miundo ya vivumishi vya Kiimenti na jinsi usarufi
unavyowakilishwa katika maumbo ya vivumishi; kupambanua ruwaza za usarufi katika
vivumishi vya Kiimenti na kutathmini sheria za mpangilio wa vivumishi katika tungo za
Kiimenti. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Sarufi Geuza Umbo Zalishi (Chomsky,
1957; 1965) na Nadharia ya Fonolojia Zalishi Asilia (Hooper, 1976). Nadharia ya Sarufi
Geuza Umbo Zalishi ilisaidia kuchanganua maumbo ya vivumishi kimofemiki huku
miundo ya nje na ndani ya vivumishi husika ikichunguzwa. Vivumishi vya Kiimenti
hupitia michakato mingi ya kifonolojia vinapodhihirisha muundo wa nje kutoka muundo
wa ndani. Nadharia ya Fonolojia Zalishi Asilia ilitumika kuchunguza michakato hiyo na
sheria zinazohusika. Uchunguzi wa nyanjani na maktabani ulifanyika. Nyanjani, utafiti
ulifanywa katika wadi ya Abothũgũchi ya Magharibi katika kaunti ndogo ya Meru ya
Kati. Mbinu ya sampuli makusudi ilitumiwa kuteua eneo la utafiti na wasailiwa
walioshirikishwa katika utafiti huu. Walengwa wa utafiti huu walikuwa wazungumzaji
wazawa wa lahaja ya Kiimenti ili kuhakikisha uthabiti wa data. Mtafiti alihudhuria
mikutano ya machifu, kanisa na ya wazazi shuleni ili kukusanya data ya vivumishi
ambayo ilichanganuliwa. Mbinu za utafiti zilizotumiwa ni kurekodi mazungumzo ya
wasailiwa katika mikutano hii kwa kutumia kalamu na karatasi pamoja na kinasa sauti
cha rununu. Aidha, tasnifu, makala mahsusi na vitabu hasa vya hadithi katika lahaja ya
Kiimenti na vingine vilivyohusu mada ya utafiti huu vilisomwa katika maktaba za vyuo
vikuu vya Kenyatta, Nairobi, Moi, Egerton na Chuka. Kazi zaidi zilisomwa katika
maktaba ya Wizara ya Elimu iliyoko jijini Nairobi ambapo tasnifu nyingi za vyuo vikuu
mbalimbali zimehifadhiwa. Data ya vivumishi vya Kiimenti iliyopatikana
ilichanganuliwa kwa kupanga aina mbalimbali za vivumishi katika majedwali na
kuondoa uradidi uliojitokeza. Kisha vivumishi husika vilifanyiwa unukuzi wa kifonetiki
na kutafsiriwa. Aidha, vilichanganuliwa ili kuamua utendakazi wa kisarufi ulioainishwa.
Hatua nyingine ilihusu kupangilia sentensi zenye mpangilio sawa wa vivumishi pamoja
na kuzifanyia unukuzi wa kifonetiki. Kisha zilitafsiriwa na sheria kuandikwa zilizodhibiti
kila ruwaza ya vivumishi katika sentensi. Utafiti ulibainisha kuwa kivumishi cha
Kiimenti huwasilisha muundo mahsusi wenye mofimu zinazotekeleza kazi za kisarufi.
Inatarajiwa kwamba utafiti huu utakuwa mchango mkubwa wa kiisimu kwa kuwasaidia
wanafunzi, walimu na watafiti wengine wakichunguza lugha za kiasili. Pia, utafiti
utasaidia katika uhifadhi wa lahaja ya Kiimenti kwa vizazi vijavyo.